Wednesday, September 08, 2010

Merkel alaani mipango ya kuchoma Koran


BERLIN

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameielezea mipango ya Kanisa moja nchini Marekani kutaka kuchoma moto Koran kuwa ni ya chuki na ambayo si sahihi. Kitendo cha Kanisa hilo lililopo Florida, kutaka kuchoma moto nakala za Koran tukufu tarehe 11 mwezi huu wa Septemba kimelaaniwa ndani na nje ya Marekani. Makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Vatican na Umoja wa Mataifa pia wamelaani mipango hiyo.
Kwa upande wake Vatican imesema mipango hiyo ni uovu na ishara mbaya dhidi ya Waislamu na kitabu chao kitakatifu. Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Eric Holder aliiita mipango hiyo ya kipumbavu na ya hatari. Kamanda wa majeshi ya Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Afghanistan, Jenerali David Petraeus, alionya kuwa mipango hiyo inaweza ikahatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani.
Wakati huo huo, Kanisa la Ujerumani lililoanzishwa na Mchungaji Terry Jones limesema mipango hiyo haihusiani na imani yao. Stephan Baar wa jumuiya ya Kikristo mjini Cologne, amesema Jones alianzisha Kanisa hilo nchini Ujerumani katika miaka ya 1980, lakini walijitenga nalo mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment